Numbers 20

Maji Kutoka Kwenye Mwamba

(Kutoka 17:1-7)

1 aKatika mwezi wa kwanza jumuiya yote ya Kiisraeli ilifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.

2 bMahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Musa na Haruni. 3 cWatu wakagombana na Musa, na kusema, “Laiti tungelikufa wakati ndugu zetu walipoanguka na kufa mbele za Bwana! 4 dKwa nini mmeileta jumuiya ya Bwana kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu? 5 eKwa nini mmetupandisha kutoka Misri mpaka mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”

6 fMusa na Haruni wakaondoka pale kwenye kusanyiko mpaka kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa Bwana ukawatokea. 7Bwana akamwambia Musa, 8 g“Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Haruni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”

9 hKwa hiyo Musa akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Bwana kama alivyomwagiza. 10 iMusa na Haruni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Musa akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” 11 jNdipo Musa akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.

12 kLakini Bwana akamwambia Musa na Haruni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”

13 lHaya yalikuwa maji ya Meriba,
Meriba maana yake Kugombana.
mahali pale ambapo Waisraeli waligombana na Bwana, naye akajionyesha mwenyewe huko kuwa mtakatifu katikati yao.

Edomu Wakatalia Israeli Kupita

14 nMusa akawatuma wajumbe kutoka Kadeshi kwenda kwa mfalme wa Edomu, akisema:

“Hili ndilo ndugu yako Israeli asemalo: Wewe unafahamu juu ya taabu zote ambazo zimetupata.

15

oBaba zetu walishuka Misri, nasi tumeishi huko miaka mingi. Wamisri walitutesa sisi na baba zetu,

16

plakini tulipomlilia Bwana, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri.

“Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako.

17

qTafadhali turuhusu tupite katika nchi yako. Hatutapita katika shamba lolote, wala shamba la mizabibu, au kunywa maji kutoka kwenye kisima chochote. Tutasafiri kufuata njia kuu ya mfalme, na hatutageuka kulia wala kushoto mpaka tuwe tumeshapita nchi yako.”

18 rLakini mfalme wa Edomu akajibu:

“Hamtapita hapa; kama mkijaribu kupita, tutatoka na kuwashambulia kwa upanga.”

19 sWaisraeli wakajibu:

“Sisi tutafuata njia kuu; tena ikiwa sisi au mifugo yetu tutakunywa tone la maji yenu, tutalilipia. Sisi tunataka tu kupita kwa miguu, wala si kitu kingine chochote.”

20Watu wa Edomu wakajibu tena:

“Hamwezi kupita hapa.”

Ndipo watu wa Edomu wakatoka dhidi ya Waisraeli, jeshi kubwa lenye nguvu.
21 tKwa kuwa Waedomu waliwakatalia Waisraeli kupita katika nchi yao, Israeli wakageuka, wakawaacha.

Kifo Cha Haruni

22 uJumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori. 23Kwenye Mlima Hori, karibu na mpaka wa Edomu, Bwana akamwambia Musa na Haruni, 24 v“Haruni atakusanywa pamoja na watu wake. Hataingia katika nchi ninayowapa Waisraeli, kwa sababu ninyi wawili mliasi dhidi ya agizo langu kwenye maji ya Meriba. 25 wWatwae Haruni na Eleazari mwanawe, na uwapandishe juu katika Mlima wa Hori. 26 xMvue Haruni mavazi yake, na umvike Eleazari mwanawe, kwa maana Haruni atakusanywa pamoja na watu wake; atakufa huko.”

27 yMusa akafanya kama Bwana alivyomwagiza: Wakapanda Mlima Hori mbele ya macho ya jumuiya yote ya Kiisraeli. 28 zMusa akamvua Haruni mavazi yake na kumvika mwanawe Eleazari mavazi hayo. Naye Haruni akafia pale juu ya mlima. Kisha Musa na Eleazari wakateremka kutoka mlimani. 29Jumuiya yote ilipofahamu kwamba Haruni amekufa, jamaa yote ya Kiisraeli wakamwomboleza kwa siku thelathini.
Copyright information for SwhKC